Waziri wa Elimu nchini Julius Migos Ogamba amevitaka vyuo vikuu nchini kuanza maandalizi ya mapema kwa ajili ya kupokea wanafunzi watakaohitimu chini ya mtaala wa CBE, ifikapo mwaka wa 2029.
Akizungumza jijini Mombasa wakati wa kufungua mkutano wa wasimamizi wakuu wa vyuo vikuu vya umma, Waziri Migos alisema wanafunzi wa mtaala huo watakuwa na ujuzi na maarifa kwenye  nyanja mbalimbali.
Aidha alisema taasisi za elimu ya juu zinapaswa kuoanisha mitaala yao na mahitaji ya mfumo huo mpya pamoja na soko la ajira.
Migos, alisisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa mitaala ya elimu ya juu ili kuhakikisha wanaohitimu wanakuwa na ushindani pamoja na uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa mara tu wanapomaliza masomo yao.
Aidha, Migos aliezihimiza taasisi hizo kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali, ili kukabiliana na changamoto za uhaba wa ufadhili na kuongeza uwekezaji katika tafiti na ubunifu.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
