Chama cha CUF Tanzania chaonya njama ya kuvurugwa kwa uchaguzi

Chama cha CUF Tanzania chaonya njama ya kuvurugwa kwa uchaguzi

Mwenyekiti wa Chama cha upinzani nchini Tanzania cha Wananchi CUF Prof Ibrahim Lipumba ametoa wito wa mchakato wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi huu nchini humo kutoingiliwa na vyombo vya dola.

Chama hicho kilimuomba Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mgombea wa Chama tawala cha CCM kuwahakikishia wananchi kwamba maoni yao yanaheshimiwa kupitia uchaguzi wa demokrasia.

Lipumba aliyewahi kuwania urais zaidi ya mara tatu amesema licha ya mazingira kutokuwa rafiki kwa vyama vya upinzani nchini humo ni lazima ukuzaji wa demokrasia kupewa kipaumbele nchini humo.

Wakati huo huo Lipumba alisema Rais Samia anapaswa kuweka mazingira ya ukweli na uwazi katika uchaguzi huo na kiongozi atakayechaguliwa anapaswa kutangazwa bila ya vyombo vingine kuingilia mchakato huo.

Hata hivyo Jeshi la Tanzania kupitia msemaji wake David Misime lilionya vikali dhidi ya wale wanaotengeneza na kusambaza taarifa za uchochezi huku akisisitiza kwamba jeshi hilo linafuatilia nyendo za wahusika na litawafikisha kwenye mkono wa sheria.

Tanzania inajiandaa na uchaguzi mkuu Oktoba 29 mwaka huu huku chama kikuu cha upinzani kikijiweka kando na uchaguzi huo, kikishinikiza kufanyika marekebisho yanayomulika mazingira ya uchaguzi.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi