Familia Yatafuta Hifadhi Nje ya Nchi yao Baada ya Ndugu Kufunguliwa Mashtaka ya Uhaini Tanzania

Familia Yatafuta Hifadhi Nje ya Nchi yao Baada ya Ndugu Kufunguliwa Mashtaka ya Uhaini Tanzania

Familia moja inatafuta hifadhi ya kisiasa nje ya nchi kufuatia kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini kwa baadhi ya wanafamilia wake nchini Tanzania, baada ya machafuko ya kisiasa yaliyojitokeza hivi karibuni. Inadai kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wao, na madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Kwa mujibu wa mwanafamilia mmoja aliyeomba kutotajwa jina, jamaa hao—Ramadhan Haruna Ramadhan na Hamis Seleman Yakub—walifunguliwa mashtaka baada ya kushiriki maandamano yaliyopinga matokeo ya uchaguzi yaliyokuwa na utata. Familia inasema ombi la hifadhi linalenga kuwalinda, ikitaja mazingira ya vitisho na sintofahamu huku mamlaka zikiendelea kutetea mashtaka ya uhaini.

Familia inaeleza kuwa kukamatwa kwao kulitokea baada ya maandamano ya Desemba 9, ambapo walichukuliwa na vikosi vya usalama. Ingawa waliachiwa huru tarehe 13 Desemba, baadaye mamlaka ziliwafungulia mashtaka rasmi ya uhaini, hatua iliyoongeza hofu ya kuendelea kunyanyaswa.

“Kwa ajili ya usalama wao, tayari tumewapeleka Ubelgiji,” alisema mwanafamilia huyo aliyeomba kutotajwa jina.

Kwa mujibu wa familia, shinikizo kutoka serikalini limeongezeka tangu mashtaka hayo yalipofunguliwa, huku vyombo vya habari vya Tanzania vikizuiwa kuripoti habari zinazohusiana na kesi hiyo.

Ikumbukwe kuwa, mahakama ya Tanzania iliwafungulia mashtaka ya uhaini angalau watu 240 kufuatia maandamano ya vurugu ya mwezi Novemba yaliyohusiana na uchaguzi wa urais.

Rais Samia Suluhu Hassan alitangazwa mshindi wa uchaguzi kwa asilimia 98 ya kura, matokeo yaliyopingwa vikali na upinzani, ambao ulizuiwa kushiriki uchaguzi huo na kuutaja kuwa wa mizaha.

Vikosi vya usalama vilikabiliana na waandamanaji waliokuwa wakipinga matokeo hayo, huku vyanzo mbalimbali vikidai kuwa mamia ya watu waliuawa. Hata hivyo, mamlaka zimepunguza ukubwa wa vurugu hizo na kusisitiza kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.

Baada ya machafuko hayo, watu kadhaa walikamatwa na sasa wamefunguliwa mashtaka ya uhaini katika mahakama iliyopo Dar es Salaam, kituo cha kibiashara cha Tanzania. Washtakiwa hawakutakiwa kuwasilisha maelezo ya kukiri au kukana mashtaka wakati wa kufikishwa mahakamani.