Bingwa wa dunia mbio za mitaa 1500 Faith Kipyegon ateuliwa kuwania tuzo za kila mwaka za ‘Laureus World Sportswoman of the Year.’

Bingwa wa dunia mbio za mitaa 1500 Faith Kipyegon ateuliwa kuwania tuzo za kila mwaka za ‘Laureus World Sportswoman of the Year.’

Nyota wa mbio za masafa ya kati kutoka Kenya, Faith Kipyegon, amepata uteuzi wake wa tatu mfululizo kuwania tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Kike wa Mwaka katika hafla maarufu ya Laureus World Sports Awards, hatua inayozidi kuthibitisha ubabe wake katika kizazi hiki cha wanariadha.

Tuzo hizo, zinazotambuliwa kimataifa kama “Oscars za Michezo”, huandaliwa na Laureus Sport for Good Foundation na hulenga kutambua mafanikio ya kipekee, uthabiti na mchango chanya wa michezo duniani.

Uteuzi wa Kipyegon kwa miaka mitatu mfululizo unaonyesha si tu kipaji chake, bali pia uimara wa kiwango chake cha juu kwa muda mrefu. Mwaka 2024 aliteuliwa baada ya msimu wa kihistoria wa 2023 ambapo alivunja rekodi tatu za dunia na kushinda dhahabu mbili katika Mashindano ya Dunia.

Mwaka 2025 alirejea tena kwenye orodha ya wateule kufuatia mafanikio makubwa katika Michezo ya Olimpiki ya Paris, ambako aliweka historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kushinda medali tatu za dhahabu mfululizo katika mbio za mita 1,500.

Sasa mwaka 2026, anawania tuzo hiyo tena baada ya kuvunja rekodi yake mwenyewe ya dunia ya mita 1,500 na kutwaa taji lake la nne la dunia katika msimu bora wa 2025.

Katika kinyang’anyiro cha mwaka huu, Kipyegon anakutana na ushindani mkali kutoka kwa nyota wengine wa kimataifa akiwemo Sydney McLaughlin-Levrone, Melissa Jefferson-Wooden, Aitana Bonmati, Aryna Sabalenka, na Katie Ledecky.

Uteuzi huu unaendeleza hadhi ya Kipyegon kama mmoja wa wanariadha bora zaidi duniani na fahari kubwa kwa Kenya katika jukwaa la kimataifa.