Bunge la Mombasa laidhinisha mswada wa mfuko wa mwaka 2025

Bunge la Mombasa laidhinisha mswada wa mfuko wa mwaka 2025

Bunge la kaunti ya Mombasa limeidhinisha mswada wa mfuko wa mzunguko wa kaunti ya Mombasa wa mwaka 2025, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati katika kaunti hiyo.

Mswada huo unapendekeza kufutwa kwa Sheria ya mfuko wa pamoja wa mzunguko ya mwaka 2016, na kuanzisha mfumo mpya wa kusimamia na kuendesha mfuko huo kwa njia iliyo wazi na yenye ufanisi zaidi.

Mwenyekiti wa kamati ya Leba na utawala wa huduma za umma katika bunge la kaunti hiyo, ambaye pia ni Mwakilishi wadi ya Mikindani Jacktone Madioalo, amesema kupitia mfumo huo mpya, serikali ya kaunti inalenga kuimarisha uwezeshaji wa kiuchumi kwa wafanyabiashara wadogo.

Kwa upande wao wajumbe wa bunge hilo wameeleza kuwa kupitia mfuko huo, wakaazi wa kaunti ya Mombasa watapata urahisi wa kupata msaada wa kifedha, huku masharti ya mikopo yakiwa rafiki na yasiowakandamiza.

Mswada huo sasa unasubiri kutiwa saini na Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sharrif Nassir ili uwe sheria.

Taarifa ya Mwanahabari wetu