Ripoti ya waangalizi wa Umoja wa Afrika imesema uchaguzi wa Tanzania uliofanyika Oktoba 29, haukuzingatia viwango vya demokrasia na kanuni za kimataifa.
Ujumbe huo ulieleza kwamba uchaguzi wa Tanzania uliyoshuhudia utata na ambao uligubikwa na maandamano, haukuzingatia kanuni za Umoja wa Afrika, mifumo ya kisheria za kimataifa kuhusu viwango vya uchaguzi wa kidemokrasia.
Katika ripoti yao ya baada ya uchaguzi, waangalizi hao wa umoja wa Afrika walisema walishuhudia masunduku yaliyojazwa kura kabla ya upigaji kura kuanza katika baadhi ya vituo na kwamba wapiga kura walipewa zaidi ya karatasi moja ya kura na wengine waliruhusiwa kupiga kura bila uthibitisho wa utambulisho wao.
Waangalizi hao wa AU walifafanua kwamba mawakala wa vyama vya kisiasa katika vituo vya kupigia kura waliwataka waangalizi hao kuondoka kwenye vituo vya kura, hali iliyozua mashaka kuhusu uadilifu wa mchakato huo.
Hata hivyo licha ya madai yaliyotolewa na ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Afrika kuhusu wizi wa kura, serikali ya Tanzania ilisema uchaguzi huo ulifanyika kwa njia huru, haki na uwazi.
Ripoti ya waangalizi wa AU inaonekana kukinzana na ujumbe wa pongezi wa Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja huo Mahmoud Ali Youssof, aliyempongeza Samia kwa kuchaguliwa tena kuiongoza Tanzania.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
