Tundu Lissu adinda kuendelea na kesi mahakamani

Tundu Lissu adinda kuendelea na kesi mahakamani

Chama cha Chadema nchini Tanzania kimedinda kuendelea na kesi ya uhainini inayomkabili mwenyekiti wake Tundu Lissu hadi pale wanachama na wafuasi wake watakapokuwa wanaruhusiwa kuingia mahakamani.

Akizungumza mbele ya majaji watatu, Lissu alisema kesi yake inapaswa kusikilizwa hadharani, lakini maafisa wa polisi wamekuwa wakiwazuia wanachama wake kuingia mahakamani.

Lissu aliiomba mahakama itoe mwongozo wa haraka, kwa kuwa ni majaji pekee walio na mamlaka ya kutoa mwongozo wowote mahakamani kwa mujibu wa sheria.

Baada ya hoja hiyo kuwasilishwa, jaji kiongozi Dastan Ndunguru aliahirisha kesi hiyo kwa muda na kusema watarejea kutoa maamuzi.

Jumatatu 14, Septemba 2025 kulitokea makabiliano kati ya baadhi ya polisi na wanachama wa Chadema nje ya mahakama.

Polisi walidai vurugu hizo zilisababishwa na wanachama waliokataa kufuata maelekezo yao.

Kesi ya Lissu inaendelea kusikilizwa katika mahakama kuu, Masijala ya Dar es Salaam, huku kampeni za uchaguzi zikiendelea.

Chama chake cha Chadema kilisema hakitashiriki uchaguzi hadi mabadiliko ya sheria za uchaguzi yatakapofanyika.

Taarifa ya Joseph Jira