Miraj, aitaka kaunti ya Mombasa kuwajibikia mafuriko

Miraj, aitaka kaunti ya Mombasa kuwajibikia mafuriko

Seneta Maalum Miraj Abdillahi amewataka wakaazi wa kaunti ya Mombasa kuchukua tahadhari ya mapema na kujiepusha na athari za mvua kubwa ambayo tayari zimesababisha vifo na uharibifu wa mali katika baadhi ya maeneo nchini.

Miraj alisema ni muhimu kwa wakaazi kuwa makini hasa katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko mara kwa mara, akiwashauri kuepuka kuvuka mito au mitaro yenye maji mengi wakati wa mvua.

Seneta huyo pia aliihimiza serikali ya kaunti ya Mombasa kuchukua hatua za haraka za kusafisha mitaro ya maji na kuondoa marundiko ya taka ambayo mara nyingi huziba na kusababisha mafuriko wakati wa mvua.

“Kuna haja ya serikali ya kaunti ya Mombasa kuweka mikakati bora ya kuzuia majanga kwa sababu kuna kitengo maalum cha kufanya hiyo kazi na wako na bajeti mbona tena hakuna hatua zozote zinazofanywa, ni wakati sasa wakuwa na fikra za kulindwa wananchi wetu dhidi ya majanga na mafuriko”, alisema Miraj.

Wakati huo huo alielezea kukerwa na changamoto za ukosefu wa umeme mara kwa mara nchini, akisema imesababisha vifo vya watoto 8, akiita idara husika kuwajibika kikamilifu.

Taarifa ya Mwanahabari wetu