Upinzani nchini Sudan Kusini ulitoa wito Jumatatu 15, Septemba 2025, wa uhamasishaji wa silaha kufanya “mabadiliko ya serikali” ili kukabiliana na mipango ya kumweka kiongozi wake mahakamani kwa makosa ya uhaini na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Mkataba dhaifu wa kugawana madaraka kati ya rais Salva Kiir na mpinzani wake wa muda mrefu, Riek Machar, umekuwa ukisuasua kwa miezi kadhaa, na kutishia kurejesha taifa hilo changa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya watu 400,000 katika miaka ya 2010.
Siku ya Alhamisi, Machar alishtakiwa kwa kosa la mauaji, uhaini na uhalifu dhidi ya ubinadamu na kuvuliwa wadhifa wake kama makamu wa kwanza wa rais katika serikali ya muungano, akiwa tayari amekaa miezi kadhaa chini ya kifungo cha nyumbani.
Alishtakiwa kwa kuamuru shambulio la wanamgambo wa kikabila kwenye kambi ya kijeshi mnamo Machi 2025, ambayo serikali ilisema iliua zaidi ya wanajeshi 250.
Mrengo wa Machar ulikanusha mashtaka hayo na ulisema ni sehemu ya juhudi za Kiir kuweka kando upinzani na kuimarisha mamlaka.
“Utawala wa sasa… ni muundo wa udikteta, wavunjifu wa amani na utekaji nyara wa serikali ambao unashikilia mamlaka kinyume cha sheria na kwa vurugu,” chama chake kilisema katika taarifa iliyotiwa saini na kaimu mwenyekiti Oyet Nathaniel Pierino na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Chama na vikosi vyake “vitafanya kazi katika Jamhuri ya Sudan Kusini mabadiliko ya serikali”, ilisema taarifa hiyo, ikitoa wito kwa wafuasi wote “kuripoti kwa Jeshi la Kitaifa ili kulinda raia na nchi”.
Sudan Kusini ilipata uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka 2011 lakini ikatumbukia katika mzozo mkubwa kati ya Kiir na Machar.
Vita vya miaka mitano vilimalizika kwa makubaliano ya amani mwaka 2018 lakini majaribio ya jumuiya ya kimataifa kuhakikisha mabadiliko ya kidemokrasia yameshindwa.
Uchaguzi uliopaswa kufanyika Desemba 2024 uliahirishwa tena hadi 2026 na pande hizo mbili hazijaunganisha vikosi vyao vya kijeshi.
Taarifa ya Joseph Jira
