Mpina apata pigo lengine la kuondolewa kwenye orodha ya wagombea wa urais Tanzania

Mpina apata pigo lengine la kuondolewa kwenye orodha ya wagombea wa urais Tanzania

Mgombea urais kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo Luhaga Joelson Mpina amekutana tena na kizingiti kingine baada ya Tume ya Uchaguzi nchini Tanzania kuondoa jina lake kwenye orodha ya wagombea wa wadhfa wa urais.

Uamuzi huo wa Tume ulitokana na pingamizi lililowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania Hamza Said Johari dhidi ya Mpina.

Mpina aliondolewa kwenye orodha ya wagombea siku nne tu baada ya kushinda kesi katika Mahakama Kuu Masjala Kuu ya Dodoma alipokuwa akipinga uamuzi wa awali wa Tume wa kumzuia kurudisha fomu ya kuteuliwa kugombea nafasi ya Urais.

Kwa mujibu wa taarifa ya ACT Wazalendo, pingamizi la Mwanasheria Mkuu wa Serikali lilidai kwamba Mpina hakuwa na sifa ya kuwa Mgombea wa Urais kufuatia uamuzi wa awali msajili wa vyama vya siasa.

Katika taarifa yake kwa umma, ACT Wazalendo kilikitupia lawama Chama Cha Mapinduzi (CCM) juu ya mapingamizi yaliyowekwa dhidi ya mgombea wake Mpina kikidai kwamba mapingamizi hayo hayakuwa na ukweli wala msingi wowote.

Haijafahamika bado ikiwa ACT Wazalendo watarudi mahakamani kupinga tena pingamizi hili jipya la Tume ya Uchaguzi au La.

Taarifa ya Elizabeth Mwende