Mahakama kuu nchini Tanzania imemrejesha kwenye debe mgombea urais wa chama cha upinzani ACT wazalendo, Luhaga Mpina na kupindua maamuzi yaliyotolewa na tume ya uchaguzi nchini humo INEC.
Hii inamaana tume ya INEC ni lazima imjumuishe Mpina katika orodha ya majina ya watakaopigiwa kura, hatua itakayosababisha upinzani kwenye uchaguzi huo mkuu.
Hatua hii sasa inampa Mpina fursa ya kuanzisha kampeni za kutaka kumbandua mamlakani rais Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Octoba 29 mwaka 2025.
Kampeni za uchaguzi tayari zinaendelea nchini humo.
INEC ilimzuia mpina kugombe wadhifa wa urais mwezi Agosti 26, 2025 ikidai chama cha ACT Wazalendo kilikiuka taratibu za chama kwa kumsimamisha Mpina kuwania wadhifa huo.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa katika kampeni za uchaguzi mkuu.
Katika uamuzi uliotolewa Alhamisi  mwezi Septemba 11, 2025, jopo la majaji watatu mjini Dodoma liliagiza INEC kumuidhinisha Mpina kama mgombea wa urais.
Anatarajiwa kujumuika na wagombea wengine 16 kutoka vyama vidogo vya kisiasa katika mapambano hayo ya kuwania urais, ambao wote wanania ya kung’atua rais wa sasa Samia Suluhu Hassan mamlakani.
Chama cha Chadema kilizuiwa kugombea katika uchaguzi huo baada ya kiongozi wake Tundu Lissu kufunguliwa mashtaka ya uhaini.

Kiongozi wa upinzani wa Chadema Tundu Lissu akiwa mahakamani.
Rais Samia Suluhu Hassan alichukua hatamu za uongozi kama rais baada ya kifo cha John Pombe Magufuli mwaka 2021.
Taarifa ya Joseph Jira.
