Mahakama ya Tanzania yazuia kesi ya Lissu kupeperushwa hewani

Mahakama ya Tanzania yazuia kesi ya Lissu kupeperushwa hewani

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA, Tundu Lissu, imezuiwa kurushwa mubashara au kuchapishwa taarifa za ushahidi baada ya Mahakama kutoa agizo maalum la kulinda mashahidi wa siri wa kiraia.

Akisoma uamuzi huo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Franko Kiswaga alisema zuio hilo lilitolewa kwa mujibu wa maelekezo ya Mahakama Kuu.

Aidha alieleza kwamba taarifa za mwenendo wa shauri hilo zitasomewa Mahakamani hadharani lakini utambulisho wa mashahidi wa siri utafichwa.

Hakimu Kiswaga pia aliagiza Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuhariri taarifa za uwasilishaji wa shauri hilo ili kuhakikisha majina na maelezo yanayoweza kumtambulisha shahidi hayatajwi.

Aliongeza kuwa mtu yeyote ikiwemo vyombo vya habari atakayetaka kuchapisha taarifa zinazohusu mashahidi atalazimika kupata kibali maalum, vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya atakayekiuka.

Katika hatua ya Jumatatu tarehe 18 Agosti 2025, Lissu atasomewa taarifa za mwenendo wa upelekeaji shauri hilo katika Mahakama Kuu, bila kuhitajika kujibu chochote kwa sasa.

Hata hivyo, nje ya mwenendo wa shauri, viongozi wa CHADEMA walilalamikia utaratibu wa ulinzi wa Mahakama, wakidai kwamba kulikuwa na idadi kubwa ya watu waliovaa kiraia ndani ya chumba cha Mahakama ambao wanaamini ni askari polisi.

Lissu anakabiliwa na mashtaka ya uhaini ambayo, endapo atahukumiwa, adhabu yake ni hukumu ya kifo.

Mpaka sasa amekaa rumande kwa zaidi ya miezi mitatu akisubiri mwenendo wa shauri kupelekwa Mahakama Kuu.

Taarifa ya Elizabeth Mwende