News
Felkin: Tumeweka mikakati ya kutoa elimu ya juu kupitia mtandao
Waziri wa Elimu kaunti ya Kilifi Felkin Kaingu alisema serikali ya kaunti ya Kilifi imeweka mikakati ya kuimarisha mpango wa elimu kwa wote unaotoa elimu ya juu kupitia mtandao.
Akizungumza na Coco Fm, Waziri Kaingu alikariri kuwa tayari serikali ya kaunti ya Kilifi imetenga bajeti ya kufanikisha utumizi wa mtandao wa bure yani Wi-Fi katika maeneo kadhaa ya kaunti.
Kaingu alisema eneo la bustani ya Mazingira mjini Kilifi, Soko la kwa Charo ya Mae, Mtwapa, Mariakani miongoni mwa maeneo mengine yaliteuliwa kuwekewa mtandao huo wa Wi-Fi.
“Tuko na mipango mizuri ya kuhakikisha tumeweka mitandao wa Wi-Fi, katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha vijana wanaweza kupata elimu kupitia mtandao”, alisema Felkin.
Waziri Kaingu alisema kuwa Gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro, anapania kuimarisha vijana kupitia mifumo mbalimbali ikiwemo elimu mtandaoni.
Waziri huyo pia alibaini kuwa watakaofuzu kupitia mpango huo wa elimu kwa wote watanufaika na ajira sio tu za humu nchini lakini pia ughaibuni.
Taarifa ya Hamis Kombe