News
Inspekta Jenerali Kanja aomba Msamaha.
Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja ameomba msamaha kwa kutoa ripoti isiyo sahihi kuhusu uchunguzi wa mauaji dhidi ya mwalimu na mwanablogu Albert Ojwang.
Mapema wiki hii, Kanja alidai kuwa Ojwang alifariki kwa kujitoa uhai baada ya kujigonga kichwa kwenye kuta za seli za polisi.
Madai hayo yalizua taharuki miongoni mwa wananchi ambao walishutumu polisi kwa kujaribu kuficha ukweli kuhusu kifo cha mwanablogu huyo.
Wakati wa kikao cha bunge la seneti siku ya jumatano tarehe 11 mwaka 2025, inspekta jenerali Kanja alilaani mauaji hayo na kudai hangeweza kutoa tamko lolote hadi mamlaka huru ya kutathmini utendakazi wa polisi (IPOA) ikamilishe uchunguzi wake.
Pia aliapa kuwachukulia hatua maafisa wa polisi waliompatia ripoti hiyo akitaja taratibu za kinidhamu zitaambatana na taratibu za kawaida za uendeshaji.
“Ikiwa katika uchunguzi unaoendelea na IPOA tutajua ukweli, maafisa waliotoa ripoti ya awali watalazimika kukabiliwa na taratibu za kinidhamu, kutokana na kile tulichosikia hapa, tutaendelea na kuchukua hatua zinazohitajika dhidi ya afisa aliyetupa nyenzo siku hiyo,” Kanja alisema.
Hata hivyo maseneta hao walipinga matamshi ya Kanja na kudokeza kuwa IPOA imefutilia mbali madai ya Ojwang’ kujiua kufuatia kutolewa kwa matokeo ya uchunguzi wa maiti.
Ripoti ya upasuaji wa maiti ya mwanapatholojia wa serikali Bernard Midia , ilithibitisha kuwa Ojwang alitendewa ukatili, kunyongwa, kuteswa na kuuawa na maafisa wa polisi.

Albert Ojwang’ mwalimu na mwanablogu anayedaiwa kuuawa na maafisa wa polisi.
Kisa cha mauaji ya mwanablogu huyo Albert Ojwang’ kilizua mihemko miongoni mwa wakenya huku baadhi ya vijana pamoja na wanaharakati wa kutetea haki za kibinadam nchini wakiandamana wakishinikiza naibu inspekta mkuu wa polisi Eliud Lagat kujiuzulu na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Taarifa ya Joseph Jira