News
Uingereza imeekeza dola milioni 60 kwa mradi wa Kawi ya jua, Kilifi
Serikali ya Uingereza ilitangaza kuekeza kima cha dola milioni 60 zaidi katika mradi wa uzalishaji wa Kawi ya miale ya jua katika eneo la Langobaya kaunti ya Kilifi.
Kulingana na Balozi wa Uingereza nchini Kenya Neil Wigan, hatua hiyo itasaidia kuongeza viwango vya uzalishaji wa kawi ya miale ya jua katika kituo hicho.
Wigan alidokeza kwamba mpango huo unalenga kuimarisha pakubwa sekta ya uwekezaji nchini hasa katika kaunti ya Kilifi.
“Tumeekeza zaidi ya dola milioni 60 kwa ajali ya kuekeza mradi huu kwani aliyekuwa akijenga mradi huo alikuwa anautekeleza kwa nafasi ndogo lakini vile tumemsaidia itafungua kazi nyingi na tunafikia kuongeza zaidi ili kufikia mega watsi 80”, alisema Wigan.

Kawi ya miale ya jua katika eneo la Langobaya, Malindi
Kauli yake imeungwa mkono na Katibu wa idara ya uekezaji nchini Abubakar Hassan ambaye amesema uzalishaji wa kawi katika kituo hicho ni hatua muhimu kwa taifa la Kenya kwani itasaidia kupunguza bei ya umeme sawa na kulinda mazingira.
Kwa upande wake Naibu Gavana wa kaunti ya Kilifi Flora Mbetsa Chibule amesema kaunti ya Kilifi kupitia uongozi wa Gavana Gedion Mung’aro inathamini sana uungwaji mkono kutoka kwa serikali ya Uingereza na hatua hiyo inaonyesha wazi ushirikiano mwema katika ya serikali ya Kenya na Uingereza.
Taarifa ya Mwanahabari wetu