Entertainment
Steven Otieno: Niliweka Video ya Kujiua WhatsApp – Ilibadilisha Maisha Yangu
Katika eneo la Mnarani, Kaunti ya Kilifi, mwanaharakati wa mazingira Stephen Otieno anasimama kama ishara ya ushindi dhidi ya changamoto za maisha. Ni hadithi ya maumivu, kimya, msongo wa mawazo – lakini pia ni simulizi ya matumaini, uponyaji, na kuibuka upya.
Kwenye mahojiano ya kusisimua katika kipindi cha Janjaruka 254, Otieno, amefungua moyo wake kwa mara ya kwanza hadharani kuhusu kipindi kigumu zaidi maishani mwake – alipokaribia kujitoa uhai.
Mizigo ya Matumaini Yasiyolingana na Uhalisia
Baada ya kumaliza masomo, wazazi wa Otieno walikuwa na matarajio makubwa kutoka kwake. Walitarajia msaada wa kifedha, msaada wa kijamii – na hata matumaini ya mafanikio ya haraka. Lakini maisha halisi yalikuwa tofauti. Kipato chake kilikuwa cha ulinzi wa usiku – kazi maarufu kama “askari gongo” – yenye malipo duni na mazingira magumu.
Wazazi wake hawakuweza kuelewa hali hiyo. Walizidi kumlilia msaada bila kufahamu kuwa hata yeye alikuwa akihangaika kuendesha maisha yake na ya mke wake, ambaye alimwoa muda mfupi baada ya kuhitimu masomo. Hilo liliwafanya wazazi wake kuchanganyikiwa zaidi – na hilo ndilo lilikuwa chanzo kikuu cha msongo wa mawazo kwa kijana huyu.
Kimya Kilichokaribia Kugharimu Maisha
Kosa kubwa ambalo Otieno anakiri ni kutoongea. Hakumweleza mtu yeyote kuhusu msukosuko huo – hata mkewe. Alibeba msalaba huo kimya kimya hadi usiku mmoja, akiwa kazini kwenye eneo lisilo na watu wengi, alipoamua kujitoa uhai. Kabla ya kuchukua hatua hiyo ya mwisho, alirekodi video na kuiweka kwenye WhatsApp status yake na kushiriki kwenye kundi moja la marafiki.
Simu zaidi ya 100 ziliingia kwa haraka – watu waliotaka kujua tatizo na kumrai asikate uhai wake. Video ile ya sekunde chache ilibadili kila kitu.
Mwanzo wa Safari ya Uponyaji
Msimamizi wake kazini alikimbia hadi eneo alilokuwepo Steven usiku huo. Ndipo Steven alipomwaga moyo wake – kwa mara ya kwanza – na kueleza hali halisi aliyokuwa nayo. Hilo ndilo lilikuwa chimbuko la safari yake mpya.
Kikao cha familia kilifanyika. Wachungaji walihusishwa. Wataalamu wa afya ya akili walimsaidia. Na kwa mara ya kwanza, jamii ilimskia – na kumwelewa. Aliambiwa kwamba hakustahili kupambana peke yake. Aliambiwa kwamba alihitaji kuongea.
Kugeuka na Kuwa Mchochezi wa Mabadiliko
Kupitia shirika la Baha Madzo Gadze for Charity, Otieno alipata nafasi ya kujitolea katika shughuli za kulinda mazingira. Alipewa majukumu madogo madogo ambayo baadaye yalikuza nafasi yake hadi kuwa Naibu Mwenyekiti, kisha Mwenyekiti wa kikundi hicho. Hapo ndipo aligundua maana ya kweli ya maisha – ya kuwa msaada kwa wengine na kwa mazingira yanayotuzunguka.
Anasema: “Sijafikia malengo yangu kikamilifu, lakini nipo kati ya asilimia 40 hadi 50. Hilo ni jambo kubwa kwa mtu aliyekaribia kujiua. Sasa naona mwangaza.”
Ujumbe kwa Wengine
Steven Otieno amebeba ujumbe mzito kwa vijana na watu wote wanaopitia msongo wa mawazo:
”Ongea na mtu. Hata kama ni mtu wa barabarani. Pigia simu mtu unayemwamini. Post kwa mitandao ya kijamii kama huna wa kuongea naye. Usijifiche. Tangamana. Utajifunza na kusaidiwa.”
Anamalizia kwa kusema:
“Bado naihifadhi ile video niliyorekodi nikitaka kujiua. Sijatamani kuifuta kwenye hifadhi zangu. Sio kwa sababu naifurahia, bali kwa sababu ni kumbukumbu ya wapi nimetoka. Leo hii, nipo hapa kwa sababu niliongea. Na nitaendelea kuzungumza ili wengine waone kuwa kuna tumaini.”
Katika ulimwengu ambapo matarajio ya jamii yanaweza kuvunja nafsi, hadithi ya Stephen Otieno ni ushuhuda wa nguvu ya mazungumzo, msaada wa kijamii, na kuamini kuwa maisha yana thamani – hata unapohisi umekwama. Leo hii, sio tu kuwa amepona, bali amegeuka kuwa sauti ya mabadiliko – kwa binadamu na mazingira.