News

Bitok: Wanafunzi wa Gredi ya 9 kutumia KEMIS kujiunga na shule za Upili

Published

on

Wanafunzi wa Gredi ya 9 watajiunga na shule za sekondari mwaka ujao kwa kutumia mfumo mpya wa kielektroniki wa kuwasajili wanafunzi maarufu kama KEMIS.

Kulingana na Katibu katika Wizara ya Elimu nchini Julius Bitok, Serikali imebuni mfumo huo wa kieletroniki ili kuhakikisha wanafunzi wote walioko Gredi ya 9 wanajiunga na shule za sekondari.

Bitok ametangaza kwamba wanafunzi milioni 1.2 walioko Gredi ya 9 watajiunga na Gredi ya 10 katika shule za sekondari mwakani.

Mfumo huo wa kieletroniki uliovumbuliwa wiki iliyopita jijini Nairobi utanakili wanafunzi wote nchini kuanzia shule za Chekechea, msingi, upili, taasisi za kiufundi na vyuo vikuu.

Awali Wizara hiyo ilikuwa ikitumia mfumo wa NEMIS kuchukua takwimu za wanafunzi katika shule za umma ili itume mgao wa fedha za elimu ya bure kisha baadaye ikabadili hadi KEMIS huku kamati ya bunge kuhusu elimu ikiongozwa na Mwenyekiti wake Julius Melly ikiunga mkono mfumo huo na kuitaka Wizara hiyo kuhakikisha inanakili wanafunzi wote nchini.

Bitok amesema kila mtoto atapata nafasi katika shule za sekondari licha ya kuwa na shule chache za sekondari nchini.

Kulingana na takwimu katika Wizara hiyo kuna shule elfu 10 za sekondari huku idadi ya wanafunzi ikiwa kubwa mno ikilinganishwa na shule za sekondari.

Taarifa ya Elizebeth Mwende

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version