News
Achani, Aagiza wizara 10 zilizogatuliwa kupeana kandarasi kwa Vijana
Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani ameagiza wizara 10 zilizogatuliwa katika serikali za kaunti kupeana kandarasi za kutekeleza miradi ya maendeleo kwa makundi ya akinamama na vijana katika kaunti hiyo ili kukabiliana na suala la ukosefu wa ajira na kupunguza viwango vya umaskini.
Kulingana na Gavana Achani, kufikia sasa jumla ya kampuni 300 za akina mama na vijana zimesajiliwa huku kampuni 105 zikipewa kandarasi za ujenzi wa zahanati, shule za Chekechea, upanuzi wa mabomba ya maji miongoni mwa kandarasi zengine.
Gavana Achani alisema hatua hiyo itasaidia wakaazi wa Kwale kujiajiri na kupunguza viwango vya umaskini.
“Nilisema akina mama na vijana waunde kampeni ili tuweze kujiajiri kwani hali ya uchumi kwa sasa hivi ni mbaya kwani saa hizi pale serikali ya kaunti imefikishwa haiwezi kuajiri na ni lazima tutafute njia mbadala za ni vipi watu watawezepata nafasi za ajira”, alisema Achani.

Kwa upande wake Katibu wa Wizara ya Huduma za Jamii na Ukuzaji Talanta katika serikali ya kaunti ya Kwale Riziki Mwasoza alisema kuwa wamekuwa wakiwapa mafunzo kina mama na vijana waliosajili kampuni na kuwajimiza kutumia kampuni hizo kusaka zabuni katika mashirika ya kibinafsi.
“Kama idara mwaka uliopita tuliwafanyia mafunzo akinamama na vijana ya siku tatu ili kujua jinsi ya kusimamia mapato yao”, alisema Mwasoza.
Nao wakaazi ambao wanamiliki kampuni na waliofaidika na kandarasi za serikali ya Kwale wakiongozwa na Mathew Kailu kutoka Shimbahills alieleza kwamba tangu wasajili kampuni hizo wamepata zabuni za hadi shilingi milioni 9 zinazowapa faida kubwa na kufanya miradi mbali mbali ya kuwajimu kimaisha.
Taarifa ya Mwanahabari wetu