News
Mwandishi wa Vitabu vya Tamthilia Ngugi wa Thiong’o amefariki
Mwandishi nguli wa vitabu vya tamthilia Ngugi wa Thiong’o ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 87.
Familia imethibitisha kifo chake kilichotokea siku ya Jumatano Mei 28, 2025 nchini Marekani.
Ngũgĩ wa Thiong’o ni mmoja wa waandishi mashuhuri na wenye ushawishi mkubwa kutoka Afrika, hasa nchini Kenya. Anafahamika sana kwa maandishi yake ya kifasihi, hasa Riwaya, Tamthilia, Insha na tafakari kuhusu Lugha, Siasa, Utamaduni na Ukoloni.
James Ngugi wa Thiong’o, baadaye alijulikana kama Ngũgĩ wa Thiong’o baada ya kuacha jina la Kikristo.
Alizaliwa tarehe 5 Januari 1938 katika kijiji cha Kamĩrĩthũ, eneo la Limuru katika kaunti ya Kiambu.
Ngugi alisoma katika shule ya upili ya Alliance High School – mojawapo ya shule za kitaifa nchini Kenya, kisha akaelekea katika chuo kikuu cha Makerere nchini Uganda na kuhitimu mwaka 1963 na akajiunga na chuo kikuu cha Leeds nchini Uingereza ambako aliendelea na masomo yake ya fasihi.
Ngũgĩ alianza kuandika vitabu katika lugha ya Kiingereza lakini baadaye aliacha kutumia Kiingereza katika kazi zake za fasihi na kuanza kuandika kwa lugha za Kikuyu na Kiswahili, kama njia ya kuendeleza utamaduni na lugha za Kiafrika.
Baadhi ya vitabu vyake maarufu ni pamoja na Weep Not, Child (1964) – riwaya ya kwanza ya Mwafrika kuchapishwa kwa Kiingereza.
Vingine ni pamoja na The River Between (1965), A Grain of Wheat (1967), Petals of Blood (1977), Devil on the Cross (Caitaani Mutharaba-ini, 1980) – aliandika akiwa gerezani, kwenye karatasi za chooni na Matigari (1986) – kitabu hiki kilipigwa marufuku Kenya kwa sababu ya ujumbe wake wa mapinduzi.
Baada ya vitisho vya kisiasa na kushambuliwa nchini Kenya, Ngũgĩ alihamia Uingereza, kisha Marekani, ambako ameendelea kufundisha katika vyuo vikuu mbalimbali hadi kifo chake.
Taarifa ya Eric Ponda