News
Mashahidi zaidi wajitokeza dhidi ya Mackenzie
Kesi dhidi ya mhubiri tata Paul Mackenzie na washukiwa wenzake 38 kuhusu ukatili na ukiukaji wa haki za watoto inaendelea kusikizwa katika mahakama ya watoto ya Tononoka, Mombasa mbele ya hakimu mkuu Nelly Chepchirchir.
Shahidi wa 43, Sajenti mwandamizi Joseph Yator, alieleza jinsi mtoto aliyenusurika kutoka Shakahola alivyoripoti kuwa watoto wawili walifunikwa nyuso na mama zao hadi kufariki baada ya kushindwa kufa kwa kufunga.
Yator alisema alipewa amri ya mahakama kufukua miili hiyo ili kubaini chanzo cha vifo hivyo, lakini baada ya Mackenzie kuachiliwa kwa dhamana ya polisi, alikuta makaburi hayo yakiwa matupu.
Aliongeza kuwa mwili mmoja kati ya hiyo miwili ulipatikana kwenye kaburi tofauti na kupelekwa kwa vipimo vya DNA, ambapo matokeo yalionyesha kufanana kwa asilimia 99 na ndugu wa familia hiyo.
Shahidi wa 44, Julius Kiprotich, alisimulia jinsi mkewe, Alice Kawira, aliyefuata mafundisho ya Mackenzie, alivyochoma vitabu na sare za shule za watoto wao, na pia kumtoa mamake hospitalini na kutupa dawa zake, akidai matibabu ni ushetani.
Kiprotich alitoa ushahidi wa kusikitisha akieleza jinsi mkeke na wafuasi wengine wa kanisa la Good News International walivyosherehekea kifo cha mtoto wao wa pili badala ya kuomboleza, baada ya mkewe kushindwa kumpeleka mtoto hospitalini.
Alieleza mahakama jinsi mkewe alivyomtoa mtoto kwa siri kutoka shule na kuhamia Shakahola na kisha kukatiza mawasiliano.
Mama yake Julius Kiprotich, Bi. Hellena, pia alithibitisha ushahidi wa mwanawe kwa kueleza kuwa Alice Kawira na Julius walikuwa wanandoa na walikuwa na watoto wawili, ushahidi wake pia uliunga mkono madai ya Julius kwamba Alice Kawira alimtoa mtoto wao shuleni Eldoret na kuhamia Malindi.