News
Polisi wamewakamata vijana sita Wahalifu, Kaunti ya Kilifi.
Maafisa wa Idara ya DCI kwa ushirikiano na kitengo maalum cha Polisi wamefanikiwa kuwakamata vijana sita wanaoshukiwa kuwa wahalifu.
Katika taarifa ya Polisi, wahalifu nao wanadaiwa kwamba wamekuwa wakiwapora wananchi fedha zao wanapozuru benki mbalimbali.
Kamanda wa Polisi eneo la Kilifi Kusini Hassan Rochale amethibitisha kukamatwa kwa wahalifu hao, akisema maafisa wa polisi wako makini kuhakikisha wahalifu wote wanakabiliwa kisheria.
Maafisa wa polisi wamesema wakati wa makabiliano na wahalifu hao, mhalifu mmoja alipigwa risasi na kujeruhiwa mkono huku magari mawili yenye nambari bandia za usajali pamoja na vifaa nyingine hatari vilivyotumika kwa uhalifu vikinaswa na maafisa wa polisi.
Aidha wamesema wahalifu hao wamekuwa wakiwahangaisha wakaazi wa kaunti za Kilifi na Mombasa, na kwamba wamekamatwa katika eneo la Kadzengo kwenye barabara kuu ya Mombasa – Malindi wakielekea maeneo ya Mtwapa kutoka Kilifi.
Wahalifu hao ni pamoja na Erick Wachira, Ali Said Nassir, Fredrick Kalugo Konde, Nicholas Mungaro Kitumba, Fred Mwajira, na Edwin Kyalo Mulandi.
Wahalifu hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kijipwa kaunti ya Kilifi wakisubiri kufikishwa Mahakamani.