Entertainment
Millennials Bongo Tour: AY Kuwasha Moto Nairobi!
Nguli wa Bongo Flava kutoka Tanzania, AY, ametua jijini Nairobi tayari kwa tamasha linalosubiriwa kwa hamu – Millennials Bongo Tour, litakalowasha moto Kilimani, Jumapili hii, tarehe 1 Juni.
AY ambaye hiyo jana ameachia vibao vipya SIMUONI na SI NDO MANAKE akishirisha na Harmonize na Darasa mtawalia, atakuwa sura ya tamasha hilo la kipekee la muziki wa Afrika Mashariki. Atasindikizwa na mwanamuziki mahiri kutoka Burundi, Kidum, pamoja na DJ Redbone wa Nairobi, anayejulikana kwa kuamsha burudani kwenye kila tamasha.
Tamasha hili linaahidi mchanganyiko wa kipekee wa vibao vya kumbukizi na ladha ya kisasa ya Bongo Flava. AY, anayejulikana kwa vibao vilivyotikisa chati kama Zigo, Touch Me Touch Me, na Microphone, amewaahidi mashabiki onyesho lisilosahaulika.
“Inahisi vizuri sana kurejea Nairobi. Nipo tayari kuwapa mashabiki wangu burudani ya kukumbukwa,” alisema AY mara baada ya kuwasili.
Kuongeza ladha ya kipekee, Kidum atapanda jukwaani na vibao vyake vya kuburudisha kama Mapenzi na Haturudi Nyuma, huku DJ Redbone akikoleza utamu kwa mchanganyiko mtamu wa Afrobeat, Bongo Flava, na nyimbo kali za ukanda huu.
Millennials Bongo Tour si tamasha la kawaida—ni sherehe ya kitamaduni inayotambua muziki wa Bongo kama daraja linalounganisha vizazi na mataifa. Toleo hili linatoa heshima kwa magwiji wa muziki wa Afrika Mashariki waliotengeneza historia na ambao wanaendelea kuwapa msukumo wasanii wapya hadi leo.
“Hili si tamasha tu—ni sherehe ya muziki wa Afrika Mashariki na fursa ya kipekee kwa mashabiki kuungana na magwiji waliounda sauti ya kizazi,” alisema mmoja wa waandaaji wa tamasha hilo.