News
Waziri Ruku, aunga mkono mswada tata wa kuzuia maandamano
Waziri wa utumishi wa umma nchini Geoffrey Ruku ameendelea kuunga mkono mswada tata wa kudhibiti mikutano na maandamano wa mwaka 2024.
Mswada huo, ambao kwa mara ya kwanza uliwasilishwa na Ruku wakati alipokuwa Mbunge wa Mbeere Kaskazini, umeibuka tena wakati huu ambapo maandamano yanayoongozwa na vijana wa kizazi cha Gen Z yanaendelea kushika kasi kote nchini.
Maandamano haya yameibua hisia kali huku vijana wakiibua masuala ya haki za binadamu, uwajibikaji wa serikali, na mustakabali wa taifa.
Waziri Ruku alitetea mswada huo, akisema kwamba mfumo wa sasa wa kisheria kuhusu mikutano na maandamano hauna nguvu za kutosha kudhibiti maandamano ya vurugu na ghasia kwani maandamano ambayo yamekuwa yakifanyika nchini yamekosa mwelekeo na uongozi thabaiti.
“Sheria ya umma ya mwaka 1952 ni ya zamani sana. Haikutungwa kwa ajili ya Kenya ya kidemokrasia na kwamba sheria mpya itanyamazisha wakenya kwa vurugu na kuwezesha maandamano ya amani, alisema Ruku.
Kulingana na Waziri huyo, mswada mpya unapendekeza kufutwa kwa sehemu ya 5 na 6 ya sheria ya agizo la umma na badala yake kuanzisha mfumo mpya wa kusimamia maandamano na mikutano ya hadhara.
Kwa mujibu wa mapendekezo ya sheria hiyo, waandamanaji watalazimika kutoa taarifa kwa polisi kati ya siku 3 hadi 14 kabla ya kufanyika kwa mkutano au maandamano yoyote.
Hata hivyo, wachanganuzi wa masuala ya kisiasa pamoja na Wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu wamekosoa vikali mswada huo, wakisema ni njama fiche ya kuzuia sauti za wananchi, hasa vijana wa kizazi cha Gen Z.
Wakosoaji hao walisema mswada huo mpya unaweza kuibua masharti magumu zaidi kwa umma kuandamana kwa amani na kwamba kuhatarisha haki ya msingi ya kujieleza na kukusanyika kwa amani.
Mswada huo unalenga kuchukua mkondo mpya baada ya Mwakilishi Kike kaunti ya Nairobi Esther Passaris kuwasilishwa mapendekezo mpya kuhusu mswada huo ambapo analenga kuzuia waandamanaji kuandamana katika maeneo yaliopigwa marufuku hasa bunge, Mahakama, ofisi kuu za umma na Ikulu pamoja na waandamanaji hao kuwa umbali wa mita 100 kutoka maeneo hayo.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi