News
Mahakama kuu yatupilia mbali ombi la Gachagua
Mahakama kuu imetupilia mbali ombi la pili la aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua la kutaka jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi ya kupinga kubanduliwa wake mamlakani kuzuiliwa kuskiza kesi hiyo.
Gachagua alisema kwamba majaji hao watatu akiwemo Jaji Eric Ogola, Anthony Mrima na Fridah Mugambi wanafaa kuondolewa kwenye kesi hiyo kwa misingi kwamba uteuzi wao haujazingatia sheria.
Mahakama hiyo ilitupilia mbali ombi hilo, na kusema kwamba jopo hilo la majaji watatu liliteuliwa na Jaji mkuu Martha Koome kwa kuambatana na sheria na kanuni za idara ya Mahakama.
Mahakama imeshikilia kwamba jopo hilo la majaji wa Mahakama kuu litaendelea kusikiliza kesi hiyo hadi wakati wa kutoa uamuzi kwa kuzingatia sheria, na kanuni za idara ya Mahakama pamoja na Katiba ya Kenya.
Mahakama hiyo pia ilitupilia mbali ombi la Mwanaharakati Fredrick Mula ambaye alitaka kubadilishwa kuwa mlalamishi katika kesi nne za kuondolewa mashtaka dhidi ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ambazo alikuwa amewasilisha awali na kisha kutaka kujiondoa.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi