News
Wakaazi Wanaotafuta Vitambulisho Wahimizwa Kufuatilia Stakabadhi hizo
Mkurugenzi wa kituo cha huduma mjini Kilifi kaunti ya Kilifi Linet Magwar amewataka wakaazi wanaotuma maombi ya kupata vitambulisho kuhakikisha wanafuatilia stakabadhi hiyo baada ya kutuma maombi.
Hii ni kufuatia mrundiko wa vitambulisho vya wakaazi wengi katika kituo hicho cha huduma kutokana na wakaazi hao kususia kuchukua vitambulisho vyao.
Magwar alisema wanalazimika kutumia maafisa tawala kuhakikisha kuwa vitambulisho hivyo vinawafikia walengwa hasa wale waliosusia kuvifuatilia katika kituo cha huduma.
Afisa huyo alisema kuna umuhimu wa wakaazi wa Kilifi pia kufahamu huduma mbalimbali ambazo hutozwa ada sawa na zile ambazo hazitozwi ada yoyote ili kuepuka kuitishwa fedha kwenye huduma zisizohitaji fedha.
Taarifa ya Hamis Kombe