News
Viongozi wahimizwa kushirikiana kubuni ajira kwa vijana
Mwakilishi wa wadi ya Sabaki eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi Rose Baraka alitoa wito kwa viongozi wa kaunti ya Kilifi kushirikiana na mashirika ya kijamii pamoja na wawekezaji katika kaunti ya Kilifi ili kudhibiti changamoto za ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.
Rose alisema hatua hiyo itasaidia pakubwa kuwaepusha vijana kujiingiza kwenye utumizi wa mihadarati sawa na uhalifu.
Akizungumza wakati wa kikao kilichowaleta pamoja maafisa wa shirika la SHOFCO pamoja na wakaazi wa Sabaki, Rose aliahidi kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kijamii katika juhudi za kuwasadia wananchi kujiendeleza kupitia mpango wa ajira.
“Vijana ni wengi, kazi ni kidogo. Sisi kama viongozi tunastahili kutia bidii kutafuta haya mashirika ili tuangalie vijana wetu wasaidika vipi’’ alisema Rose Baraka.
Kwa upande wake Afisa wa Shirika la SHOFCO eneo la Magarini Kelvin Mtawali Karisa aliupongeza ushirikiano wa mwakilishi wa wadi huyo na shirika hilo na kuwataka vijana kujiunga kwenye makundi mbalimbali ili waweze kupata mikopo ya kujiendeleza kimaisha.
Taarifa ya Janet Mumbi