News
Wakaazi Kilifi washinikiza serikali kukusanya maoni kabla miradi kuanza.
Serikali kuu imeandaa kikao cha kukusanya maoni ya umma pamoja na wadau mbali mbali kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya kitaifa kaunti ya Kilifi katika chuo kikuu cha pwani.
Akizungumza katika kikao hicho katibu mkuu wa maswala ya uratibu katika ofisi ya mkuu wa mawaziri Ahmed Abdisalam, alisema kikao hicho kinatoa fursa kwa wananchi kufahamu namna serikali inavyotekeleza miradi yake kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Abdisalam aliongeza kuwa wananchi wanamchango mkubwa katika kutambua changamoto zozote zinazojitokeza kwenye mchakato wa utekelezaji wa miradi hiyo, akidokeza kuwa kaunti ya kilifi ni miongoni mwa kaunti zinazofaidi miradi mingi ya serikali.
“Tunataka kuhakikisha tunatembea na wananchi kutoka hatua ya kutambua miradi, utekelezaji na pia inapokamilika, malengo ni kusistiza uhusika wa wananchi ili kuwa na uendelevu wakati wa kutekeleza miradi ya serikali kuu”, alisema Abdisalam.
Kwa upande wake kamishna wa kaunti ya Kilifi Josephat Biwot alidokeza kuwa serikali kwa sasa inaendeleza miradi mbali ikiwepo ujenzi wa nyumba za bei nafuu eneo la Tezo na Mtwapa pamoja na ujenzi wa soko eneo la Watamu.
Biwot vile vile alisema serikali inajenga vyumba vya malazi ya zaidi ya wanafunzi 1,700 katika chuo kikuu cha pwani pamoja na ujenzi wa barabara ya Bamba kuelekea Ganze huku ile ya Mwakirunge ikitarajiwa kuanza karibuni.
“Tuko na miradi mipya iliyoanzishwa na serikali iliyomamlakani kama ujenzi ya nyumba za bei nafuu, tuko na miradi wa Tezo na Mtwapa ambayo inaendelea na pia tuko na ujenzi wa masoko unaendelea, watamu liko zaidi ya asilimia 70 kukamilika”, alisema kamishna Biwot.
Kwa upande wao baadhi ya wanachi waliohudhuria kikao hicho waliikata serikali kuhakikisha inahusisha wananchi kabla miradi kuanza kutekelezwa, wakidai serikali imekuwa ikitafuta maoni ya umma wakati miradi ikiendelea.
Taarifa ya Joseph Jira