Business

Wafanyabiashara Kilifi Walalamikia Ubomozi wa Vibanda Kupisha Ujenzi wa Barabara

Published

on

Wafanyabiashara katika eneo la Misufini kuelekea Kwa Mwango, mjini Kilifi, wameelezea hofu yao kuhusu hatma ya biashara zao kufuatia tangazo la serikali ya kaunti ya Kilifi la kubomoa vibanda katika eneo hilo ili kupisha ujenzi wa barabara mpya.

Wakiongozwa na Isaac Thomas, mfanyabiashara wa bidhaa za rehani, wamesema kuwa mpango huo wa ubomoaji utasababisha hasara kubwa kwao, hasa kupoteza wateja wa kudumu, jambo ambalo linaweza kusambaratisha kabisa biashara zao.

“Biashara hii ndiyo tegemeo langu pekee. Nikiondolewa hapa bila mpango mbadala, nitapoteza wateja wangu na maisha yatakuwa magumu,” alisema Thomas.

Wameiomba serikali ya kaunti kuwapatia eneo mbadala la kufanyia biashara kabla ya kutekeleza zoezi hilo la ubomoaji, wakisisitiza kuwa wengi wao hutegemea biashara hizo kwa riziki ya kila siku.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa serikali ya kaunti, barabara inayopangwa kujengwa kutoka Misufini hadi Kibaoni inapita katika kiwanja kinachomilikiwa na Chuo Kikuu cha Pwani, hali inayowalazimu kuondoa miundo mbinu isiyo rasmi ili kuwezesha ujenzi huo.

Wafanyabiashara sasa wanasubiri kauli ya mwisho kutoka kwa mamlaka husika kuhusu mustakabali wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version