News

Wabunge washinikiza sheria mpya ya kuwakabili waandamanaji.

Published

on

Wabunge wanaharakisha mchakato wakutunga sheria inayolenga kuwakinga wao wenyewe na taasisi nyingine za serikali dhidi ya athari za maandamano ya umma siku zijazo.

Katika mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya utaratibu wa umma (Sura ya 56), mwakilishi wakike kaunti ya Nairobi Esther Passaris anataka kuwazuia waandamanaji kukusanyika ndani ya mita 100 za maeneo yaliyohifadhiwa, ikiwemo majengo ya bunge.

Pendekezo lake lililenga kuweka maeneo yaliyotengwa kwa uwazi, ya makutano na maandamano ambamo mikutano ya hadhara na maandamano yanaweza kufanyika, kulingana na Kifungu cha 37 cha Katiba.

Passaris pia ilishinikiza marekebisho ya kifungu cha 2 cha Sheria ya utaratibu wa umma ili kufafanua upya maneno “mkutano wa hadhara” na “maandamano ya hadhara.”

Zaidi ya hayo, alipendekeza kujumuisha ufafanuzi wa “mji mkuu,” “mji,” “eneo la mijini,” na “eneo la kusanyiko na maandamano.”

“Kifungu cha 5B kilichopendekezwa kinakataza kufanya mkutano wa hadhara au maandamano ndani ya eneo la mita 100 kutoka eneo la bunge, kama ilivyoelezwa chini ya sheria ya mamlaka na haki za bunge, maeneo yaliyohifadhiwa chini ya sheria ya maeneo yanayolindwa, na majengo yenye vyumba vya mahakama,” alisema Passaris.

Mwakilishi wakike kaunti ya Nairobi Esther Passaris katika hafla ya awali.(Picha kwa hisani)

Ukiukaji wa kifungu hiki utachukuliwa kuwa kosa linaloadhibiwa kwa faini isiyozidi shilingi 100,000, kifungo cha hadi miezi mitatu, au zote mbili.

Akiwa mbele ya kamati ya bunge kuhusu  usalama na utawala, Passaris alitetea pendekezo lake, akisema halilengi kukiuka uhuru wa kujieleza bali ni kuhakikisha maandamano yanafanyika kwa utaratibu.

“Utaratibu sio adui wa demokrasia, lakini msingi wake. Ninaiomba kamati kuunga mkono mswada huu – sio kwa serikali, sio kwa bunge, lakini kwa kenya,” aliongeza Passaris.

“Nilipofikiria kuhusu sheria hii, nia yangu ilikuwa kulinda utakatifu wa taasisi zinazotuweka pamoja,” aliongeza.

Hata hivyo, pendekezo hilo liligawanya kamati,baadhi ya wanachama walitoa wasiwasi kuhusu athari zake kwa uhuru wa raia.

Mwakilishi wa kike kaunti ya Kisumu Rosa Buyu alitilia shaka athari zinazoweza kutokea kwa haki ya kusikilizwa, akibainisha kuwa mara nyingi maandamano hutokea wakati wananchi wanahisi kutosikilizwa na wanahitaji kueleza hadharani kutoridhika.

Taarifa ya Joseph Jira

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version