Trump kuongoza droo ya Kombe la Dunia Washington Leo

Trump kuongoza droo ya Kombe la Dunia Washington Leo

Rais Donald Trump bado anaonekana kutokuwa na uhakika kwamba aite mchezo huo soccer au football. Lakini lengo lake huwa sahihi zaidi anapotumia mchezo unaopendwa zaidi duniani kufikia malengo ya kidiplomasia.

Trump anatarajiwa kufanya hivyo tena Ijumaa atakapokutana na viongozi wa wenyeji wenza wa Kombe la Dunia 2026 — Canada na Mexico — wakati wa droo ya michuano hiyo jijini Washington.

Kwa kuwa hili ndilo Kombe la Dunia la kwanza kuwahi kuandaliwa na nchi tatu kwa wakati mmoja, linapaswa kuwa nafasi ya pekee kuonyesha umoja wa Amerika Kaskazini, huku viongozi wote watatu wakiripotiwa kushiriki kwenye droo ya sherehe.

Lakini msimamo mkali wa Trump dhidi ya washirika wake kuhusu biashara, uhamiaji na biashara ya dawa za kulevya tangu alipochaguliwa tena madarakani unamaanisha kutakuwa na masuala mazito ya kujadili pembeni mwa hafla hiyo.

Kwa Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum, hii itakuwa mara yake ya kwanza kukutana na Trump. Aliwaambia waandishi wa habari kuwa watazungumzia biashara baina ya nchi hizo wakati wa “mkutano mfupi” kabla ya droo ambapo timu 48 zitakazokuwa zimefuzu zitagawanywa katika makundi 12 ya Kombe la Dunia.

Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney tayari ametembelea Ikulu mara mbili, lakini hii itakuwa mara yake ya kwanza kukutana na Trump tangu walipokutana kwa kifupi Korea Kusini Novemba, baada ya Trump kusitisha mazungumzo ya kibiashara kufuatia malumbano ya kushangaza kuhusu tangazo dhidi ya ushuru wa forodha.

Ofisi ya Carney iliileza AFP Alhamisi kuwa watakuwa na “mkutano mfupi wakati watakapokuwa pamoja katika Kituo cha Kennedy,” eneo litakalotumika kwa droo ya michuano, na kuongeza kuwa atakutana pia kwa kifupi na Sheinbaum.

Trump ameweka ushuru mkali kwa bidhaa kutoka Canada na Mexico ambazo haziko chini ya mkataba wa kibiashara USMCA, ambao Washington inapanga kuupitia upya mwakani.

Ametishia adhabu zaidi endapo nchi hizo zitashindwa kudhibiti uhamiaji wa kuvuka mipaka na biashara ya dawa za kulevya — na akamkera Sheinbaum kwa kudai kuwa angekuwa “sawa” na mashambulizi ya anga nchini Mexico kupambana na wauza dawa.

Wakati huohuo, Canada ilikasirishwa na mwito wa Trump mapema mwaka huu akitaka iwe jimboni la 51 la Marekani.

– ‘Tuzo ya amani’ ya FIFA –

Hata hivyo, nchi hizi tatu sasa zinajiandaa kuwa wenyeji wa tukio kubwa zaidi la michezo duniani, baada ya kuwasilisha ombi la pamoja mwaka 2017 wakati wa muhula wa kwanza wa Trump Ikulu ya White House.

Trump ametumia Kombe la Dunia bila kusita kujipatia pointi za kisiasa na kidiplomasia — ingawa uelewa wake wa mchezo huo mzuri unatokana zaidi na mwanawe Barron, mwenye umri wa miaka 19.

Rais huyo wa Marekani amekuwa na urafiki wa karibu na rais wa FIFA Gianni Infantino, ambaye pia ana uhusiano wa karibu na viongozi kadhaa wa kiimla wakiwemo Vladimir Putin wa Russia.

Trump hata alidokeza kuwa fursa ya Russia kushiriki Kombe la Dunia 2026 — licha ya kupigwa marufuku tangu uvamizi wa Ukraine 2022 — ingeweza kuwa “msukumo” kwa Moscow kukomesha vita.