Wanafunzi wa gredi ya kumi wanatarajiwa kuanza rasmi masomo yao wiki ijayo kufuatia kusambazwa kwa vitabu kwa shule za sekondari ya juu kote nchini.
Taasisi ya mtaala nchini KICD na wizara ya elimu zilisema kuwa wachapishaji vitabu tayari wamechapisha vitabu na kusambaza asilimia 50 ya vifaa vya masomo.
Afisa mkuu wa KICD profesa Charles Ong’ondo alisema jumla ya vitabu milioni 11.87 vinahitajika kwa mwaka huu wa kwanza wa elimu ya shule ya upili.
Uchapishaji na usambazaji wa vitabu hivyo umecheleweshwa kwa miezi kadhaa kufuatia mvutano kati ya wizara na wachapishaji kuhusu madeni ya shilingi bilioni 11 ambayo yalikuwa hayajalipwa.
Hata hivyo serikali ililipa sehemu ya deni hilo na kuwezesha wachapishaji kuanza kazi yao muhimu.
Waziri wa elimu nchini Julius Migos Ogamba alidokeza kuwa shughuli za masomo zitaendeshwa kwa njia iliyosawa na bila matatizo.
Taarifa ya Joseph Jira
