KPA kuanzisha ofisi ya uhusiano Kigali, Rwanda

KPA kuanzisha ofisi ya uhusiano Kigali, Rwanda

Serikali ya Kenya na Rwanda zimesaini mkataba wa makubaliano (MoU) unaolenga kuanza rasmi utekelezaji wa ofisi ya uhusiano ya halmashauri ya bandari nchini (KPA) jijini Kigali, Rwanda.

Hafla hiyo imeongozwa na katibu Mkuu wa idara ya uchukuzi nchini Mohamed Daghar, pamoja na katibu mkuu wa wizara ya miundombinu nchini Rwanda, CPA Canoth Manishimwe.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Daghar alisema makubaliano hayo yanaashiria dhamira ya pamoja ya nchi hizo mbili, kuimarisha ushirikiano wa kikanda, biashara na nafasi yao kimkakati katika sekta ya usafirishaji wa mizigo baharini na nchi kavu Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, katibu mkuu wa Rwanda CPA Manishimwe alisema KPA ina mchango mkubwa katika kurahisisha biashara ya kikanda na kusaidia wafanyabiashara wa Rwanda na kwamba kuanzishwa kwa ofisi ya KPA Kigali kutarahisisha na kupunguza gharama za kutoa mizigo, huku wateja wakiweza kufanya taratibu nyingi wakiwa majumbani mwao.

Mkurugenzi Mkuu wa halmashauri ya bandari nchini KPA nahodha William Ruto, alisisitiza juhudi zinazoendelea za kuboresha shughuli za bandari, kuongeza uwezo na kuimarisha utoaji wa huduma akisema Rwanda inaendelea kuwa mojawapo ya masoko makubwa ya mizigo inayopita katika Bandari ya Mombasa, ambapo mwaka 2025 soko hilo lilikua kwa asilimia 22 sawa na tani 156,107.

Taarifa ya mwanahabari wetu.