Taifa la Norway limefuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 1998 baada ya Erling Haaland kufunga tena katika ushindi mnono wa 4-1 dhidi ya Italia siku ya Jumapili, ushindi uliowapa nafasi ya kushiriki fainali za msimu ujao zitakazofanyika Marekani, Kanada na Mexico.
Haaland alifunga bao muhimu mara mbili ndani ya sekunde chache katika Uwanja wa San Siro uliokuwa ukimwaga mvua, na Norway wakamaliza Kundi I wakiwa na alama 24 kamili kutokana na mechi zao nane za kufuzu.
Norway ingehitaji kufungwa kwa tofauti ya mabao tisa au zaidi ili kupitwa na Italia kwa nafasi ya moja kwa moja ya kufuzu, lakini kikosi cha Stale Solbakken kilimaliza kampeni yao kwa njia ya kuvutia mbele ya mashabiki 70,000.
Hata hivyo, Solbakken hakutaka kutoa ubashiri kuhusu nafasi ya kikosi chake chenye nguvu baada ya kutamatisha ukame wa miaka 28.
“Hebu tusubiri ratiba ya makundi kwanza… sijaifikiria hata. Kwangu mimi, leo ilikuwa kuanzia asilimia 99 hadi 100, na sasa tumefanikisha kwa njia nzuri,” Solbakken aliwaambia wanahabari.
“Tusubiri tuone droo italeta nini kabla ya kuingia kwenye maswali hayo.”
Baba yake Haaland, Alf-Inge, bado alikuwa mchezaji wa timu ya taifa wakati Norway ilipocheza Kombe la Dunia mara ya mwisho miaka 27 iliyopita, mashindano yaliyotwaliwa na Ufaransa ya Zinedine Zidane.
Na mshambuliaji huyo wa Manchester City—aliyeitwa “mashine ya mabao” na Solbakken—atakua mmoja wa wachezaji wa kuangaliwa Amerika Kaskazini baada ya kufunga mabao 16 katika hatua ya kufuzu.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 ana wastani wa zaidi ya bao moja kwa kila mchezo msimu huu kwa klabu na nchi, na alikuwa mwandishi wa mabao kwa ustadi mkubwa alipopewa nafasi ya kuiweka Norway mbele kisha kuongeza bao la pili dakika ya 78 na 79.
Norway wazama Italia
Pio Esposito aliifungia Italia bao la kuongoza dakika ya 11, lakini mara tu Antonio Nusa aliposawazisha kwa shuti kali dakika ya 63, kulionekana wazi kuwa timu moja tu ingeibuka mshindi—na bao la kuvutia la Jorgen Strand Larsen dakika za nyongeza likaimaliza Italia.
Italia sasa wataelekea hatua ya mchujo mwezi Machi baada ya kumaliza kundi wakiwa nyuma ya Norway kwa alama sita na baada ya kupokea vipigo viwili vizito kutoka kwa Norway. Mashabiki wachache wa nyumbani waliobaki walipiga kelele za kuwazomea wachezaji walipotoka uwanjani San Siro.
Kocha Gennaro Gattuso aliwaomba radhi mashabiki kupitia mahojiano mafupi kwenye kituo cha RAI, na alionyesha wazi wasiwasi wake kuhusu kuporomoka kwa kikosi chake katika kipindi cha pili.
“Ni jambo linalotia wasiwasi, ningekuwa muongo nisingesema hivyo, kwa sababu unapokuwa na usiku kama huu ni rahisi zaidi kama mko pamoja na kuboresha siku hadi siku,” alisema Gattuso.
“Kinachonitia wasiwasi ni kwamba tutakutana tena baada ya miezi mitatu.”
Jitihada za Italia kufuzu moja kwa moja zilitetereka tangu mechi yao ya ufunguzi dhidi ya Norway, walipofungwa 3-0, matokeo yaliyomfanya Luciano Spalletti kuondolewa kama kocha.
Tangu Gattuso apewe timu, Azzurri wameimarika, lakini hakuna mchezaji katika kikosi chao aliye na ubora wa Haaland—jambo la kusikitisha kwa taifa lililowahi kutoa baadhi ya wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea duniani.
