News
Spika Teddy, adai wabunge wa kitaifa wanachangia kutimuliwa kwake ofisini
Spika wa bunge la kaunti ya Kilifi Teddy Mwambire ameibua madai kwamba baadhi ya wabunge wa kitaifa kutoka kaunti ya Kilifi ndio ambao wanaendeleza njama ya kumuondoa kama spika wa bunge hilo.
Kupitia video ambayo imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, Spika Mwambire alisema viongozi hao wameshirikiana na baadhi ya Wawakilishi wa wadi wa bunge la kaunti ya Kilifi ili kuhakikisha wanafanikiwa kumbandua mamlakani.
Mwambire alisema viongozi pamoja na gavana wa kaunti ya Kilifi Gedion Maitha Mung’aro wako na njama fiche ili kuhakikisha wanatimiza malengo yao ilhali hakuna sababu zozote za kimsingi.
Aidha, Mwambire alisema hadi kufikia sasa hajajua sababu kuu ambazo zinasababisha kutaka kumbandua kama Spika wa bunge la kaunti ya Kilifi.
Vilevile, alisema hatajiuzulu kama spika wa bunge la kaunti ya Kilifi na kuwakosoa wanaomtaka kuomba msamaha bila kumfahamisha makosa yake.
Taarifa ya Janet Mumbi