News
Seneta Madzayo amuonya Inspekta jenerali wa Polisi.
Seneta wa kaunti ya Kilifi Stewart Madzayo amemtaka inspekta jenerali wa polisi nchini Douglas Kanja kuhakikisha maandamano ya vijana wa rika la Gen z tarehe 25 mwezi juni 2025 hayashuhudii umwagikaji damu.
Madzayo ambaye pia ni kiongozi wa wachache katika bunge la seneti alimtaka Inspekta Kanja kuhakikisha maafisa wa polisi wanawalinda waandamanaji badala ya kuwadhuru.
Akizungumza eneo la Mzambarauni-Mtwapa eneo bunge la Kilifi Kusini, Madzayo alidokeza kuwa maandamano hayo yatakuwa ya amani akikumbusha vijana hao wa Gen Z kuhakikisha wanadumisha amani wakati wa maandamano hayo.
“Tumeskia tarehe 25 kutakuwa na maandamano ya amani, nataka kumwambia inspekta jenerali Kanja, tafadhali watoto wetu watakuwa katika maandamano ya amani kwa hivyo usijaribu hata kidogo kutumia polisi vibaya kuweza kuumiza watoto wetu”, alisema Madzayo.
Kwa upande wake mbunge wa eneo hilo Ken Chonga aliwaomba viongozi wa kanisa nchini kuombea taifa kutokana na visa vya mauaji na utekeji nyara vinavyoshuhudiwa nchini.
“Tumekuwa na changamoto kubwa sana kati ya upinzani na serikali hali ya maafa ikiingia, haya yote ambayo yanaendelea sa hii yote sababu ni siasa, langu ni kusihi kwanza kanisa tunahitaji maombi yenu”, alisistiza Chonga.
Maandamano hayo ya GEN Z yanatarajiwa kufanyika tarehe 25 mwezi juni 2025 kukumbuka vijana waliopoteza maisha wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha mwezi juni mwaka 2024.
Taarifa ya Joseph Jira