News
Serikali yafidia wakaazi wa mzozo wa Wanyamapori milioni 60
Serikali ya kitaifa kupitia Wizara ya Utalii na wanyamapori nchini imetoa kima cha shilingi milioni 60 za fidia kwa wakaazi walioathirika na mizozo ya wanyamapori katika kaunti ya Kilifi.
Akizungumza wakati wa hafla ya kutoa fedha hizo katika wadi ya Marafa eneo bunge la Magarini, Waziri wa Utalii nchini Rebecca Miano alisema fedha hizo zitafidia visa zaidi ya 1,300 vya watu walioathirika na mizozo hiyo tangu mwaka 2021 kaunti ya Kilifi.
Miano alikariri kwamba mizozo ya Wanyamapori kaunti ya Kilifi imeathiri sana maeneo ya Magarini, Ganze na Vitengeni na kuchangia uharibifu wa mimea na hata maafa, akidai kwamba serikali imeweka mikakati kabambe ya kukomesha mizozo hiyo.
Kwa upande wake Naibu gavana wa Kilifi Flora Chibule alielezea matumaini ya kupatikana kwa suluhu la kudumu kwa mizozo hiyo hasa kutokana na mikakati iliyowekwa na serikali ili kutatua suala hilo.
Viongozi na wakaazi katika mkutano wa fidia ya wanyamapori
Wakati huo huo serikali imefichua kuwa imeweka kikosi maalum cha dharura cha maafisa wanaoshughulikia visa vya uvamizi wa wanyamapori kaunti ya Kilifi ikilenga kukabiliana na visa hivyo ili kulinda maisha ya wakaazi.
Haya yanajiri huku tayari serikali ya kitaifa ikiwa imetoa jumla ya shilingi bilioni 2.8 kote nchini za fidia kwa wananchi walioathiriwa na wanyamapori katika awamu ya kwanza huku shilingi bilioni 1.36 zikitarajiwa kutolewa siku zijazo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu