Entertainment

Ronald Fenty, Baba wa Rihanna, Afariki Dunia Akiwa na Miaka 70

Published

on

Mwanamuziki maarufu duniani, Rihanna, anaomboleza kifo cha baba yake mpendwa, Ronald Fenty, aliyefariki dunia Mei 31, 2025 huko Los Angeles, Marekani, akiwa na umri wa miaka 70, baada ya kuugua kwa kipindi kifupi.

Taarifa hizo za kuhuzunisha ziliripotiwa kwa mara ya kwanza na kituo cha habari cha Starcom Network cha Barbado.

Ingawa chanzo rasmi cha kifo bado hakijatangazwa, vyanzo vya karibu vimeripoti kuwa Fenty aliaga dunia akiwa amezungukwa na familia yake, wakiwemo Rihanna pamoja na kaka yake mdogo Rajad Fenty, katika Hospitali ya Cedars-Sinai wakati wa saa zake za mwisho.

Kwa mujibu wa TMZ, Rajad alionekana akifika hospitalini mnamo Mei 28, na inadaiwa kuwa Rihanna pia alikuwa kwenye gari hilo, japokuwa hakuonekana kwenye picha.

Ronald Fenty alizaliwa mwaka 1954 huko Barbados na alikuwa msimamizi wa ghala. Alikuwa baba wa watoto sita, wakiwemo Rihanna (jina kamili Robyn Rihanna Fenty), Rajad, na Rorrey, aliowapata na aliyekuwa mke wake Monica Braithwaite, ambaye walitalikiana mwaka 2002.

Aidha, Fenty alikuwa na watoto wengine watatu—Samantha, Kandy, na Jamie—kutoka mahusiano ya awali. Familia ya Rihanna iliishi maisha ya kawaida katika nyumba ya kupangisha eneo la Bridgetown, ambalo sasa linajulikana kama Rihanna Drive. Ingawa uhusiano wa Rihanna na baba yake ulikuwa na changamoto nyingi, Fenty alihusika pakubwa katika kuhamasisha kipaji chake cha muziki tangu akiwa mdogo.

Kwa sasa, mashabiki, watu mashuhuri, na familia ya karibu wanaendelea kumpa Rihanna pole na kumfariji wakati huu wa huzuni kuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version