News
Ripoti ya upasuaji:Wakili Mathew Kyalo Mbobu alipigwa risasi mara nane
Ripoti ya upasuaji wa maiti kuhusu kifo cha wakili Mathew Kyalo Mbobu imebaini alipigwa risasi mara nane katika tukio la uvamizi ambalo lilisababisha kifo chake.
Kulingana na mpasuaji mkuu wa serikali Dkt. Johansen Oduor, risasi mbili zimepatikana zikiwa zingali mwilini, moja ikiwa imekwama kwenye uti wa mgongo.
Oduor alidokeza kuwa uvamizi huo ulitekelezwa kwa maksudi na kwa karibu zaidi ambapo risasi nyingi zilimpiga upande wake wa kulia.
Oduor vile vile alifichua kuwa majeraha kwenye sehemu ya shingo na uti wa mgongo yalisababisha uvujaji wa damu nyingi hali iliyochangia kifo.
Awali spika wa bunge la seneti Amason Kingi aligiza asasi za usalama kufanya uchunguzi wa haraka kufuatia kifo cha wakili Mbobu.
Kingi alimtaja mauaji ya wakili huyo kama yakinyama huku akimtaja wakili Mbobu kama mtu jasiri na aliyejitolea kuhudumia raia.
Wakili huyo alifariki baada ya kupigwa risasi jioni siku ya jumanne tarehe 9 Septemba 2025, akiwa katika gari lake kwenye barabara ya Lang’ata.
Taarifa za polisi zilisema mwathiriwa alipigwa risasi na watu waliokuwa kwenye pikipiki muda mfupi baada ya saa moja na nusu usiku.
Ilisemekana wakili huyo alikuwa akiendesha gari kuelekea nyumbani wakati mshambuliaji aliposimamisha pikipiki kando ya gari lake na kufyatua risasi kabla ya kuondoka kwa kasi.
Taarifa ya Joseph Jira