News
Rais Ruto kuelekea nchini Uhispania na Uingereza
Rais William Ruto anatarajiwa kuondoka humu nchini na kuelekea nchini Uhispania na Uingereza kwa ziara ya kiserikali.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Rais na kutiwa saini na Msemaji wa Ikulu Hussein Mohammed, Rais Ruto anatarajiwa kuondoka nchini leo Jumapili Juni, 29 na kuwasili katika jiji la Seville nchini Uhispania.
Katika taifa hilo, Kiongozi wa nchi amepangiwa kuhudhuria Kongamano la Nne la kimataifa la ufadhili wa Maendeleo ambapo viongozi mbalimbali wa kimataifa wataangazia kanuni mpya za ufadhili wa maendeleo.
Rais Ruto anatarajiwa kutetea kufufuliwa kwa mfumo wa kimataifa wa kushughulilia masuala ya muda mrefu kama vile umaskini uliokithiri, kuongezeka kwa ukosefu wa usawa na msukosuko wa kiuchumi pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa na upotevu wa viumbe hai.
Rais Ruto pia ataongoza kikao cha ngazi ya juu wakati wa Kongamano hilo na kufanya mazungumzo na marais wa mataifa mbalimbali pamoja na Waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez na Mfalme Felipe wa Sita.
Hata hivyo baadaye ataelekea nchini Uingereza ambapo atatia saini ubai mpya wa kimkakati baina ya Kenya na Uingereza uliowekwa ili kufungua uwekezaji, kubuni nafasi za ajira na kukuza ushindani wa kimataifa wa Kenya katika biashara, hali ya hewa, teknolojia na usalama.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi