News
Ofisi za Shule ya Wavulana ya Kinango zimeteketea
Baadhi ya ofisi za Shule ya Wavulana ya Kinango kaunti ya Kwale zimeteketea baada ya moto kuzuka katika shuleni hiyo usiku wa kuamkia siku ya Jumatano.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Siasa Mwafungo alieleza kwamba licha ya chanzo cha moto huo bado hakijabainika huenda baadhi ya wanafunzi waliotaka kwenda kwa likizo ya sikukuu ya Eid-Ul-Adha walihusika katika mkasa huo.
Mwafun go alisema kwamba moto huo uliweza kudhibitiwa japo kiasi cha mali ya thamani ya pesa imeteketea ikiwemo vitabu na vifaa vingine wanavyotumia walimu kufanya kazi zao.
“Bado tunachunguza chanzo cha moto huo lakini kiasi cha mali ya thamani ya shule imepotea kufuatia mkasa huu wa moto, maafisa wa polisi watatueleza zaidi baada ya uchunguzi kukamilika”, alisema Mwalimu mkuu.
Mwalimu huyo mkuu aliwaonya wanafunzi kwamba yeyote atakayepatikana kuhusika na mkasa huo basi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ili iwe funzo kwa wanafunzi wengine wenye utovu wa nidhamu.
“Wanafunzi tumewaonya kwamba iwapo tutabaini kwamba wamehusika katika mkasa huu basi sheria lazima itachukua mkondo wake”, alisema Mwafungo.
Wakati huo huo aliwataka wazazi wa shule hiyo kutoa shaka kwani usalama wa wanafunzi umeimarishwa huku maafisa wa upelelezi wa jinai nchini DCI katika eneo bunge la Kinango wakifanya jitihada za kubaini chanzo cha moto huo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu