Wanahabari waadhimisha siku ya Redio duniani

Wanahabari waadhimisha siku ya Redio duniani

Ulimwengu unaadhimisha Siku ya Redio Duniani huku Wanahabari eneo la Pwani wakiungana na mataifa mengine ulimwenguni kusherehekea siku hiyo.

Siku hii muhimu ya kutambua nafasi muhimu ya chombo cha Redio ambacho kinafahamika kwa kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha jamii.

Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika jijini Mombasa, ambapo Wanahabari walifanya matembezi ya amani kutoka eneo la Mapembeni hadi uwanja wa Burhani, ambako sherehe rasmi ziliandaliwa.

Mbali na matembezi hayo, Wanahabari walishiriki michezo ya kirafiki ya Soka kwa lengo la kuimarisha mshikamano ambapo Wanahabari wa redio watachuana na wale wa mtandaoni huku Wanahabari wa runinga wakimenyana na wenzao wa vyombo vya uchapishaji.

Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika chini ya kauli mbiu, redio na Akili Mnemba (AI), kuelekeza mustakabali wa utangazaji na uandishi wa hadithi, ikilenga kuangazia mchango wa teknolojia ya akili bandia katika kuboresha utangazaji na uwasilishaji wa habari.

Wanahabari wamesisitiza kuwa licha ya mageuzi ya kidijitali, redio bado ni sauti ya jamii na daraja muhimu la mawasiliano, hasa katika maeneo ya mashinani.

Taarifa ya Joseph Jira