Serikali yatenga milioni 838 kufidia waathiriwa wa soko la Mtwapa

Serikali yatenga milioni 838 kufidia waathiriwa wa soko la Mtwapa

Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya fidia ya ardhi na shilingi milioni 838 kwa kuhamisha wafanyabiashara katika eneo la Mtwapa ili kufanikisha ujenzi wa barabara ya Mombasa–Kilifi.

Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa Daraja la Mtwapa, Waziri wa Uchukuzi Davis Chirchir alisema wafanyibiashara ambao wanaendeleza biashara zao katika soko la Mtwapa watahamishwa katika maeneo mengine ambapo wataweza kuendeleza biashara zao ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, wafanyabiashara walioko katika mji wa Mtwapa ambao wameathiriwa na upanuzi wa barabara wamepewa notisi ya siku 30 kuondoka ili kupisha kuanza kwa awamu inayofuata ya ujenzi, akieleza kuwa fedha zilizotengwa zinalenga kuhakikisha uhamishaji huo unafanyika kwa utaratibu unaozingatia sheria.

Aidha  Chirchir aliongeza kuwa mradi  unaendelea vyema, akisema kuwa ukikamilika utainua uchumi wa wafanyibiashara na  eneo la Pwani kwa ujmla.

“Serikali imetenga shilingi milioni 838 zitakazohakikisha kuwa wafanyibiashara wanahamishwa katika njia nzuri  na mazingira mazuri ili kupisha ujenzi wa barabara hivyo wafanyibiashara wote msiwe na wasiwasi wowote maana mikakati imewekwa.” alisema Chirchir.

Taarifa ya Pauline Mwango