Wanahabari katika eneo la Pwani hii leo wanatarajiwa kushiriki michezo ya kirafiki ya soka kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani.
Michuano hiyo itaandaliwa katika uwanja wa Serani, kaunti ya Mombasa, ambapo wanahabari wa redio watashuka dimbani kumenyana na wenzao wa mitandaoni, huku wanahabari wa runinga wakipimana ubabe na wale wa vyombo vya uchapishaji.
Nahodha wa timu ya wanahabari wa redio Mark Mutuku amesema kikosi chake kiko imara na kimefanya maandalizi ya kutosha kwa lengo la kuhakikisha wanaadhimisha siku hiyo kwa ushindi.
“Ni siku kubwa kwetu, tumejianda kwa mechi hiyo ya kusherehekea siku ya Radio duniani sisi tuko sawa na kikosi chetu kupata ushindi.”
Naye nahodha wa timu ya wanahabari wa mitandaoni David Otieno amesema kuwa michuano hiyo si ya ushindani pekee bali inalenga kuimarisha mshikamano na umoja miongoni mwa wanahabari wa eneo la Pwani.
“So leo tumejipanga ili kupata ushindi katika mechi hiyo manake kuna kitu ambacho tunashindania,wanahabari wengi walianza kwa Radio kabila ya kuvuka kwa TV kwa hiyo ni siku kubwa kwetu kutangana nje ya chumba cha kazi.”
Otieno ameongeza kuwa kupitia michezo hiyo, wanahabari wanapata fursa ya kuungana nje ya mazingira ya kazi na kujenga mahusiano bora yatakayochangia taaluma ya habari katika eneo hilo.
Maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani huangazia mchango wa redio katika kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha jamii, huku kaulimbiu ya mwaka huu ikilenga kuangazia mustakabali wa utangazaji katika enzi ya teknolojia ya kisasa.
Wanahabari Mombasa washiriki mchezo wa Soka kusherehekea Siku ya Radio Duniani
