Serikali inasema itawachukulia hatua walimu ambao walikosa kuweka wazi idadi ya wanafunzi shuleni mwao, ikibaini kwamba shule za humu nchini zina wanafunzi hewa laki tisa.
Wizara ya Elimu nchini na Tume ya kuwaajiri walimu nchini TSC pamoja na ofisi ya mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa jinai DCI, wameanza mchakato wa kuwaadhibu au kuwafungulia mashtaka maafisa wa elimu 62, wakiwemo walimu wakuu 14.
Waziri wa wa Elimu nchini Julius Migos Ogamba alisema uchunguzi umebaini kuwepo tofauti kubwa kati ya idadi iliyoko kwenye mfumo wa elimu wa NEMIS na idadi halisi ya wanafunzi waliopatikana shuleni.
Katika shule za msingi, wanafunzi laki nane walikosekana shuleni ilhali data zao ziko kwenye mfumo wa NEMIS, na katika shule za Junior Secondary wanafunzi waliosajiliwa walikuwa laki tano zaidi ya wale walioko kwenye mfumo huo.
Ogamba alidokeza kwamba ripoti hiyo imekabidhiwa Tume ya TSC pamoja na ofisi ya mkurugenzi wa upelelezi wa jinai DCI ili kuwachukulia hatua maafisa hao wa elimu, kwa kosa la kukosa kuwasilisha data, vile vile kuwasilisha idadi ya wanafunzi bandia.
“Tumeanza uchunguzi kwa walimu wakuu 20 walioshinda kutuma data za wanafunzi na iwapo watapatikana na hatia watachukuliwa hatua, hii mambo ya wanafunzi hewa ni lazima tukomeshe”, alisema Ogamba.
Taarifa ya Joseph Jira
