News
Mbunge wa Kilifi kaszkazini Owen Baya alaumiwa na wanaharakati.
Wanaharakati wa kupambana na utumizi wa dawa za kulevya kanda ya pwani wamemkosoa mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya kutokana na hatua ya kuondoa hoja bungeni ya kupinga biashara ya zao la Mugoka.
Wakiongozwa na Famau Mohammed Famau, wanaharakati hao walisema uraibu wa mugoka umeendelea kuathiri maisha ya vijana wengi pwani na walikuwa na matumaini na mbunge huyo kukomboa maisha ya vijana kupitia hoja hiyo.
Famau alimshauri Baya kutowasilisha barua rasmi ya kuhakiki kuondoa hoja hiyo bungeni, ila kuendelea na harakati za kupambana na uraibu wa mugoka na kukomboa maisha ya vijana wa pwani.
“Mheshimiwa Baya alipochukuwa mswada huu kuupeleka bungeni sisi tulifurahi sana na kumpongeza, na hivi sasa kuuondosha bungeni tumekasirika na amefanya jambo la aibu ambalo halingefaa kufanywa na kiongozi kama yeye”, alisema Famau.
Kwa upande wake afisa mratibu mipango katika shirika la Kenya Muslim Youth alliance Asili Randani, aliitaka serikali kuu kuhusisha vijana katika miradi inayoendelea ili kuwaepusha na uhaba wa ajira unaoshuhudiwa miongoni mwao.
“Hapa eneo bunge la Kilifi kaskazini kunajanga kubwa la matumizi ya dawa za kulevya, miradi hii ingehusisha jamii moja kwa moja vijana wetu wasinge kuwa katika swala lile, vijana wakula mugoka wengi wao wamepoteza mwelekeo na wamekuwa wazembe”, alisema Randani.
Afisa mratibu mipango katika shirika la Kenya Muslim Youth alliance Asili Randani akizungumza na wanahabari Kilifi
Itakumbukwa mapema mwaka jana wa 2024 baadhi ya magavana eneo la pwani walipiga marufuku biashara ya zao la mugoka japo vita hivyo havikufaulu.
Taarifa ya Joseph Jira.