News
Mahakama ya Upeo yafutilia mbali mkataba wa kampuni ya familia ya Joho na KPA
Mahakama ya Upeo imesitisha ujenzi wa kituo cha pili cha kushughulikia nafaka katika bandari ya Mombasa baada ya kutangaza zabuni iliyotolewa na Mamlaka ya bandari nchini KPA kwa kampuni ya Portside Freight Terminals Limited kuwa kinyume cha sheria.
Jopo la majaji watano wa Mahakama ya upeo wakiongozwa na Naibu Jaji mkuu Philomena Mwilu, na Majaji Mohammed Ibrahim, Isaac Lenaola, William Ouko, na Smokin Wanjala, walibatilisha uamuzi wa Mahakama ya rufaa na kumua kwamba ulikosea kuunga mkono utumizi wa utaratibu maalum wa ununuzi chini ya kifungu cha 144A cha ununuzi wa umma (PPAD) 2015.
“Uamuzi wa KPA kuipa kampuni ya Portside Freight Terminals Limited leseni ya kuanzisha kituo cha pili cha kushughulikia nafaka kupitia utaratibu maalum wa ununuzi ulioidhinishwa haukuendana na vifungu 10(2)(c), 201(a), na 227(1) vya Katiba,” jopo linaloongozwa na Mwilu lilieleza.
Uamuzi wa Mahakama hiyo unafuatia rufaa iliyowasilishwa na Seneta wa Busia Okiya Omtatah, pamoja na Muungano wa makuli bandarini.
Walijaribu kuzuia kampuni ya Portside Freight Terminals Limited na washirika wake, Portside CfS Limited na Heartland Terminals Limited, kujenga kituo cha kushughulikia nafaka katika gati ya kisiwani- G-Section, ambayo ni sehemu ya ardhi inayomilikiwa na mamlaka ya KPA.
Taarifa ya Joseph Jira