News
Maambukizi ya Homa ya Chikungunya Yaripotiwa Mombasa
Maafisa wa afya katika kaunti ya Mombasa wamethibitisha kuwepo na mkurupuko wa ugonjwa wa Chikungunya huku zaidi ya wakaazi 25 wakiripotiwa kuambukizwa.
Kwa mujibu wa maafisa hao, mkurupuko wa ugonjwa huo umetokana na mvua nyingi inayoendelea kunyesha kaunti hiyo ambayo imepelekea kuongezeka kwa mbu ambao wanasambaza virusi vya maradhi hayo.
Kaimu mkurugenzi wa idara ya afya ya umma kaunti ya Mombasa, Aisha Wayua, alisema kwamba serikali ya kaunti tayari imeanza kuchukua hatua mbalimbali ili kudhibiti kusambaa zaidi kwa maambukizi.
“Kama nilivyotaja kulingana na takwimu ni kwamba mwaka jana hatukuwa na visa vingi vya maambukizi ya Chikungunya kwa hivyo mwaka huu hasa msimu huu wa mvua ndio tunashuhudia visa vingi ya Chikungunya na ndio maana tumekuwa tukichukua sampuli ili kuzifanyia uchunguzi wa Vinasaba katika maabara ya KEMRI”, alisema Wayua
Visa vya maambukizi vimeripotiwa katika maeneo ya Likoni, Mvita, Kisauni na Nyali huku wakaazi wakihimizwa kuchukua tahadhari ili kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa huo.
“Tumekuwa na homa ya Malaria na Dengu, watu wengi wana ufahamu kuhusu maumivu ya viungo na haya maambukizi labda ni yanakuja pamoja na viungo kuvimba, maumivu kuongezeka na pia mwili kuwa na vipele, labda ndio maana watu wamefikiria ni maradhi mapya”, aliongeza Wayua.
Taarifa ya Mwanahabari wetu.