News
KRA Yatangaza Ongezeko la Ukusanyaji wa Mapato
Licha ya hali ngumu za kiuchumi zinazoendelea kushuhudiwa nchini, Mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini KRA imetangaza kuongezeka kwa mapato yaliokusanywa mwaka wa kifedha 2024/2025 ikilinganishwa na mwaka wa kifedha 2023/2024.
KRA inasema kumekuwa na ongezeko la asilimia 6.8 la ukusanyaji wa ushuru katika mwaka wa kifedha 2024/2025.
Hii ni baada ya KRA kukusanya ushuru wa trilioni 2.61 ikilinganishwa na trilioni 2.40 zilizokusanywa mwaka wa kifedha uliopita.
KRA imeeleza pia imepitisha makadirio ya ukusanyaji wake wa ushuru kwani iliweka makadirio ya kukusanya ushuru wa kiasi cha trilioni 2.56 na kuishia kukusanya trilioni 2.61.
Ukusanyaji wa ushuru katika mashirika ya kiserikali pia umekua kwa kiwango kikubwa huku kodi za ndani kwa ndani kwenye biashara zikiendelea kuongezeka kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa KRA.
Katika ubadilishanaji wa sarafu, Mamlaka hiyo ya ukusanyaji ushuru imesema kuwa shilingi ya Kenya dhidi ya dola ya Marekani pia imeimarika ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka wa kifedha uliopita.
KRA sasa inaeleza matumaini ya kuongezeka kwa ukusanyaji wa ushuru katika mwaka wa kifedha ulioanza wa 2025/2026.