News
Mung’aro: Ushirikiano wa viongozi utaimarisha muundomsingi
Ushirikiano baina ya viongozi wa kaunti ya Kilifi na serikali kuu kupitia Wizara ya madini na raslimali za baharini umepelekea kuimarika kwa miundo msingi eneo la Jaribuni, Ganze kaunti ya Kilifi.
Haya ni kwa mujibu wa viongozi wa Kilifi wakiongozwa na Gavana Gideon Maitha Mung’aro.
Wakizungumza katika mkutano uliowaleta pamoja wawekezaji wa timbo na wakaazi katika uwanja wa Mbudzi Dispensary, viongozi hao walisisitiza haja ya wawekezaji hao kuwajibika vilivyo.
“Hakuna kazi yoyote ya timbo itakayoendelea hadi barabara imalizwe” alisema Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro.
Ni kauli iliyoungwa mkono na Mwakilishi wa Kike kaunti ya Kilifi, Getrude Mbeyu alisema kuwa wawekezaji ambao bado hawajakamilisha majukumu yao ya ujenzi wa barabara wanachangia kuzuia wenzao wasiendeleze shughuli zao uchimbaji madini.
Serikali ya kaunti ya Kilifi kwa ushirikiano na serikali kuu ilitoa amri kwa wawekezaji hao kujenga barabara hiyo kutoka Jaribuni hadi Dzitsoni ili kuwaepusha wakaazi dhidi ya vumbi.
Hata hivyo wawekazaji hao waliagizwa kujenga barabara hiyo kwa ushirikiano ambapo kufikia sasa ni mwekezaji mmoja pekee ambaye amekamilisha ujenzi huo eneo la Marere huku wengine wakisalia kujikokota.
Taarifa ya Hamis Kombe