News
Murkomen: Polisi kupokea nyongeza ya mshahara
Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen amesema serikali inalenga kufanikisha nyongeza ya mishahara ya maafisa wa polisi kote nchini kwa asilimia 10.
Waziri Murkomen alisema mpango huo utatekelezwa kwa awamu na kwa kuambatana na bajeti ya serikali ya mwaka wa kifedha wa 2025/2026 ili kuwapa motisha maafisa wa polisi na kufanikisha utendakazi bora.
Akizungumza katika kaunti ya Nandi wakati wa kikao cha baraza la usalama maarufu Jukwaa la usalama, Waziri Murkomen aliwataka maafisa wa polisi kuwa na subra wakati suala hilo linaposhughulikiwa.
“Serikali iko na mpango maalum wa kuhakikisha maaskari wetu wanapokea nyongeza ya mishahara kwa asilimia 10 na hii ni kuhakikisha tunawapa motisha maafisa wetu wa usalama na nitekelezwa kupitia Ofisi ya huduma ya polisi nchini na ile ya Inspekta jenerali wa polisi”, alisema Murkomen.
Waziri Murkomen alidokeza kwamba tatizo la majangili katika maeneo ya Pokot Magharibi, Turkana, Samburu, Baringo, na Elgeyo Markwet kama changamoto kuu ya kiuslama katika maeneo ya Bonde la Ufa, akisema serikali inafuatilia kati ya bunduki haramu elfu 5 hadi elfu 10 zinazomilikiwa na majangali.
“Tuko na tatizo kubwa katika maeneo ya bonde la Ufa hasa Pokot Magharibi na kule Baringo na Samburu lakini tumejipanga kama idara ya usalama tutahakikisha kumesambaratisha hao majangili na kurudisha bundiki zote haramu ambazo wanatumia kuhangaisha watu”, alieleza Murkomen.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi